Tabia Ya Kutaka Kumdhibiti Mwenza
Husababisha Migogoro Ya Kimapenzi
Fahamu viashiria vya tabia hiyo,vyanzo vya tabia hiyo na ufumbuzi wake
migogoro ya kimapenzi yenye kujirudia rudia huwa inajitokeza pale ambapo
mwanaume au mwanamke anachukua jukumu la mzazi wa mwenza.Kwa maana inaitwa
parenting your partner kwa maana ya tabia ya kumchukulia mwenza wako kama vile
ni mtoto mdogo hivyo muda wote unakuwa unamrekebisha tabia na kumuelekeza nini
cha kufanya.
badala ya mahusiano kuhusisha watu wawili wenye akili timamu inakuwa kinyume
chake inakuwa mama-mtoto au baba-mtoto .
Mwanamke anachukua tabia ya mama mzazi au mwanaume anachukua tabia ya baba
mzazi mahusiano yanakuwa na taswira ya mzazi-mtoto badala ya mke-mume.
katika mahusiano haya Mwanamke au mwanaume anajiona malaika,anajiona
mkamilifu,anajiona mwerevu sana,anajiona hana dosari yoyote kisha mwenza wake
anaonekana mjinga, anaonekana mzembe, anaonekana hajielewi saa 24.
VIASHIRIA VYA MWANAUME/MWANAMKE MWENYE TABIA YA KUTAKA KUM-CONTROL MWENZA WAKE
KATIKA MAHUSIANO NI:
Viashiria vya mwanaume au mwanamke ambaye
anataka KUM-CONTROL mwenza wake ni kama ifuatavyo:
1. KUMKOSOA MARA KWA MARA
Kama utakuwa na tabia ya kutaka KUM-CONTROL mwenza wako au Mwenza wako yupo na
tabia ya kutaka kukucontrol ataonyesha tabia zifuatazo.
Ikiwa wewe ndiyo mkosoaji kupitiliza juu ya tabia za mwenza wako utaona
viashiria vifuatavyo
-Unamkosoa mwenza wako kwenye kila kitu utakosoa muonekano, lafudhi,harufu ya
mwili, matumizi ya fedha, utembeaji wake, uvaaji wake,utakosoa marafiki zake,
vipaumbele vyake,tabia zake, elimu yake,utakosoa kazi yake,
-utakuwa unapata hasira kupitiliza mara kwa mara ukimuona mwenza wako kwa
sababu utamuona mkosaji saa 24,makosa ya mwenza wako ni kama vile kuchelewa
kurudi nyumbani,kutumia simu muda wote,usafi, uvaaji,afya yake na namna
anakabiliana na matatizo yake binafsi,
mara kwa mara utamuona mwenza wako hana tabia nzuri inayokufaa ukiwa mbele ya
marafiki zako pamoja na ndugu zako,mara kwa mara utamuona mwenza wako
anakuaibisha tu,hauwezi kuona jema lolote kwa mwenza wako.
Tabia ya kumkosoa mara kwa mara inaweza kusababisha muanze majibizano, kupeana
kashfa na tuhuma za usaliti, kutishiana kuachana, kutukanana, kudharauliana,
kushutumiana, kugombana,kuitana majina ya wanyama kama vile “mbwa”,kuambiana
maneno makali sana kama vile “hauna akili” mara kwa mara.
2. KUBEBA MAJUKUMU YA MWENZA WAKO
Kama utakuwa na tabia ya kutaka KUM-CONTROL mwenza wako au mwenza wako yupo na
tabia ya kutaka kukucontrol utaona mambo yafuatayo.
kwa mfano wewe ni Mwanamke unaweza kufanya kazi za usafi nyumbani ,kulea
watoto,kupika,kufua, kuuguza wagonjwa nyumbani,kulipa ada za watoto
shuleni,kulipa kodi ya nyumba au utajenga nyumba kwa gharama zako tu,utasimamia
kazi au biashara wewe pekeako wakati huohuo upo na mwanaume ndani ambaye hana
kazi,hana biashara, hajishughulishi kwa chochote,hana MSAADA wowote kwako,hana
MSAADA wowote kwa watoto,mwanaume akipewa mtaji anakula, akitafutiwa kazi
anatafuta kisingizio cha kuacha kazi,akipata fedha anakwenda kuhonga au kunywa
pombe mpaka zinaisha pesa zote anarudi nyumbani kukaa.
mwanaume akija nyumbani kazi yake kuuliza chakula akikuta hakuna chakula
anaanza kufoka, kutukana, kutoa vitisho, kuvunjavunja vitu, kukugombeza,
kukudhalilisha, kukujibu vibaya, kukushambulia kwa maneno makali sana,kusema
“hauna akili” mara kwa mara,kusema unatoa harufu mbaya sehemu za siri
mara kwa mara baada ya ugomvi anataka unyumba kwa nguvu.
inapotokea hali kama hiyo na wewe ni Mwanamke ni wazi kwamba mahusiano yenu
yamebadilika kutoka mke-mume mpaka yamekuwa mama-mtoto.
kwa maana umekuwa mama mzazi kwa huyo mwenza wako.
3. UNATAKA KUMBADILISHA TABIA
Kiashiria tosha kwamba mahusiano yenu yamebadilika kutoka mke-mume mpaka
yamekuwa mama-mtoto ni kwamba unataka kumbadilisha tabia mwenza wako.
mwanaume anapotaka kumbadilisha tabia mwenza wake huonyesha tabia zifuatazo
badala ya mwanaume kuvutiwa kimapenzi na Mwanamke mwenye hulka ya kike kama
huruma, kujali, kunyenyekea, kusamehe makosa, uvumilivu,kujitoa
,kukufurahisha,kudeka,inakuwa kinyume chake mwanaume anajikuta anavutiwa
kimapenzi na Mwanamke mwenye hulka ya ubabe, ukali kupitiliza, kiburi,
majivuno, jeuri na dharau, Mwanamke anakuwa mjuaji sana, anakuwa na misimamo
mikali sana,anakuwa haambiliki, hashauriki, anakuwa hataki kuambiwa makosa yake,
hataki kukosolewa, hataki kupangiwa cha kufanya,siku zote Mwanamke anajiona
mkamilifu, anajiona mwerevu sana, anajiona malaika, anajiona ni mzuri sana.
kisha mwanaume anajichanganya kwa kuamua kuogopa kukwazana naye, kumnyenyekea,
kuomba msamaha saa 24,kupiga magoti mara kwa mara, kumbembeleza mara kwa
mara,kuruka kupishana naye kauli,kutumia fedha nyingi sana kwa ajili ya
kumsomesha, kumfungulia biashara, kumtafutia kazi, kumnunulia zawadi za gharama
kubwa sana,kumchukulia mkopo,kulea watoto ambao Mwanamke huyo anakuwa
ametelekezwa nao.
Mwanamke anapotaka kumbadilisha mwanaume tabia atajikuta kwenye hali kama
ifuatavyo
mwanamke anajikuta anavutiwa kimapenzi na mwanaume ambaye hana hisia naye,yaani
mwanaume hamtaki Mwanamke lakini Mwanamke anakuwa king’ang’anizi,Mwanamke
anapigwa bila kosa lolote lakini anaomba msamaha,mwanaume hana kazi,hana
biashara, hajishughulishi kwa chochote, hataki kukosolewa wala hataki kuambiwa
mapungufu yake,mwanaume anakuwa na hasira kupitiliza na misimamo mikali sana
(rigid),mwanaume anakuwa amezaa watoto wengi kila mtoto na mama yake lakini
hahudumii chochote wakati huohuo Mwanamke huyo anakuwa anataka kutegesha
ujauzito ili amlazimishe mwanaume huyo amuoe wajenge naye familia lakini
mwanaume anakuwa hataki.
Mwanamke anakwenda mbali anamchukulia mkopo,anajenga ,anamfungulia
biashara,anamtafutia kazi yote hayo anafanya lakini anashindwa kujizuia.
4. HUZUNI NA UPWEKE KUPITILIZA
kiashiria tosha kwamba mahusiano yenu yamebadilika kutoka mke-mume mpaka
yamekuwa mama-mtoto ni kwamba hauna furaha hata kidogo na mara kwa mara
unajikuta upo na hasira,moyo kwenda mbio, kizunguzungu, kichefuchefu,hisia za
kisasi, kupoteza hamu ya kula, kupoteza nguvu za kufanya kazi,kutamani kujiua
au kumdhuru mwenza wako,tumbo kuvurugika,kuumwa kichwa na mgongo,kujikuta upo
na chuki na kinyongo moyoni.
5. MNAGOMBANA MARA KWA MARA
Kiashiria tosha kwamba mahusiano yenu yamebadilika kutoka mke-mume mpaka yamekuwa
mama-mtoto ni kwamba ugomvi na mwenza wako ni matukio ya kila siku.
kwa maana hamuwezi kumalizia masaa mawili bila ugomvi ,mara kwa mara mnapishana
kauli kwa vitu vidogo vidogo sana mpaka mnaanza majibizano, kupeana kashfa na
tuhuma za usaliti, kutishiana kuachana, kutukanana, kudharauliana,
kushutumiana,kuitana majina ya wanyama kama mbwa,
6. UMEANZA KUJITENGA NAYE
Kiashiria tosha kwamba mahusiano yenu yamebadilika kutoka mke-mume mpaka
yamekuwa mama-mtoto ni kwamba unajisikia upweke kupitiliza ukiwa na mwenza
wako.
Kila unapotaka kujenga ukaribu na mwenza wako unaibuka ugomvi mkubwa sana kisha
kila mtu anaondoka akiwa na hasira kupitiliza juu ya mwenza wake
VYANZO VYA KUTAKA KUM-CONTROL MWENZA WAKO NI:
Sababu za kutaka kumbadilisha tabia mwenza wako ni kama vile:
1. KULELEWA BILA BABA NDANI YA FAMILIA.
Sababu
za kumkosa baba ndani ya familia ni kifo, talaka, kutengana kwa wazazi
kutekelezwa,baba kukataa ujauzito,baba kufungwa gerezani,baba kusafiri safiri
hivyo unakuwa haujui majukumu ya baba na haujui majukumu ya mama.
Ukiwa mwanaume unakuwa haujui majukumu yako ni yapi kama mwanaume vilevile
unakuwa haujui majukumu ya mwenza wako ni yapi..
vilevile kwa Mwanamke ambaye amekuwa bila baba anakuwa hajui sifa nzuri za baba
wa kujenga naye familia,hivyo kila mwanaume ilimradi anapumua anamkubali.
Madhara yake mwanaume anakuwa hataki kulea watoto,hataki kujenga familia hapo
Mwanamke anatumia nguvu nyingi sana kumshawishi mwanaume ampende.
wakati huohuo Mwanamke anakuwa hana hisia zozote kwa mwanaume mpambanaji,muwajibikaji
kwa sababu Mwanamke anakuwa hajiamini wala hana imani kama anaweza kustahili
kupata mwanaume ambaye anajielewa.
2. KULELEWA NA BABA DIKTETA
Mwanamke ambaye amekulia familia yenye baba dikteta wapo huanza tabia ya ubabe,
ukali kupitiliza, kiburi, majivuno, jeuri, ujuaji, misimamo mikali sana na
hasira kupitiliza kama njia ya kujilinda dhidi ya vipigo vya baba.
Hivyo Mwanamke huyu akiwa mkubwa hawezi kukubali kuongozwa na mwanaume wala
kupangiwa cha kufanya badala yake atakuwa tayari kuzaa na waume za watu au wale
wanaume player boys ambao wanampa mimba na kumtelekeza bila huduma zozote kwa
sababu hapo atakuwa na uhuru wa kuishi anavyotaka.
mwanaume ambaye baba alikuwa dikteta huamua kuwa jeuri, kuonyesha dharau,
kiburi,ubabe na misimamo mikali sana hivyo anakuwa hana huruma kwa Mwanamke
,japokuwa wapo wanaume huamua kuwa kinyume chake ambapo wanakuwa na tabia ya
upole, huruma, kujali, kunyenyekea, kusamehe makosa, uvumilivu, kujitoa mhanga
kuwafurahisha wanawake wenye tabia za ubabe, ukali kupitiliza, kiburi,
majivuno, jeuri na dharau.
Hivyo mwanaume mpole kupitiliza huwa anachanganyikiwa wapi anakosea lakini
hapati jibu.
3. KULELEWA NA BABA LEGELEGE
Wapo wanaume ambao tangu utotoni hawana ujasiri wa kufanya kazi yoyote,wanakuwa
marioo,wanakuwa vibenteni kwa sababu tangu utotoni wamezoea kula bure,kuvaa
bure,kila kitu wanapewa bure hivyo hawajui majukumu yao mpaka uzeeni kwa
mwanaume wa aina hii anaweza kuzaa watoto wengi lakini hatoi huduma zozote,hata
akiwa na fedha hatoi huduma zozote kwa sababu amezoea kufanyiwa kila kitu.
wanawake ambao wamekuwa na baba legelege huzoea kuishi maisha ya uhuru
uliopitiliza hivyo hawawezi kukubali kuongozwa na mwanaume ambaye anajielewa
badala yake wao wanavutiwa kimapenzi na wanaume wapenda starehe , lakini
wakipewa ujauzito na kutekelezwa huanza kutafuta mwanaume mpole kupitiliza alee
watoto wasiokuwa wa kwake.
4. KUPUUZWA NA KUPITIA MANYANYASO
Baadhi ya watu huwa na huruma kupitiliza kwa sababu wamepitia vipigo, matusi,
unyanyasaji, udhalilishaji,kwa miaka mingi sana hivyo mpaka ukubwani hawana
uwezo wa kutofautisha mwanaume mzuri yupo na mbaya yupo au Mwanamke mzuri
yupoje na mbaya yupoje hivyo wao kuvumilia wanaona ni njia ya kudumisha
mahusiano.