Mke
wako si malaika; kuna wakati atafanya makosa mbele ya ndugu zako. Kama mume,
wajibu wako wa kwanza ni kumlinda mke wako dhidi ya ndugu zako. Ikiwa amekosea
au ukiona wanamvamia kwa maneno, kumuongelea vibaya, badala ya kuingia na
kuchangia, kumponda, au kuongeza maneno mabaya, mlinde.
Simama upande wake, na wakati mwingine jifanye kana kwamba wewe ndiye
unayependa hali hiyo. Kwa mfano, labda anavaa nguo ambazo kwenu hazikubaliki.
Badala ya kuanza kumporomoshea maneno kama, “Huyu mwanamke kiburi sana,
nishamuambia asitukalie uchi!” ongea nao kwa utulivu. Waambie, “Mimi
ndiye nampenda, ni mke wangu, na ninafurahia jinsi alivyo.” Kwa mfano:
“Hizo nguo ni uamuzi wangu, na mimi sina tatizo.”
Hata kama hupendi, mbele ya ndugu zako waoneshe kwamba wewe ndiye unayesimamia
familia yako. Ndugu zako wakuone wewe ndiyo una shida. Baada ya hapo, ukiingia
chumbani, mweleze mke wako kwa utulivu, “Zile nguo sitaki kuziona tena.
Umeniaibisha mbele za watu.” Akianza kuhoji, kama vile: “Si
ulinitetea?” mjibu: “Nilikutetea kwa sababu ni wajibu wangu kama mume
wako, lakini pia ni lazima uheshimu familia yangu.”
Akizidi kufanya hivyo, chukua hatua ya kubadilisha vitu vyake polepole, na
wengine waone mabadiliko ili wajue ni wewe umeamua, si yeye.
Acha tabia ya kutangaza matatizo ya mke wako kwa watu. Sio uanaume, na mara
nyingi watu wanakudharau wewe kwa kuonekana huwezi kumlinda au kumdhibiti mke
wako, badala ya kumlaumu mke wako. Heshimu ndoa yako kwa kuhakikisha kuwa
migogoro yenu inabaki ndani ya ndoa!