Clickable WP Image

LOOH DADA MARTHA

JOIN US WHATSAPP CLICK HERE
JOIN US TELEGRAM CLICK HERE

Sehemu Ya 26

ILIPOISHIA

:“Mimi na Martha wajina wangu, nani unampenda zaidi?”

“Martha wewe.”

“Basi mtumie meseji kwamba umeamua kuwa na mimi, hivyo jioni utakwenda kuchukua nguo zako tu.”

“Mh! Atakuibulia ugomvi wewe.”

“Mimi nipo tayari.”

Wakati wakizungumza hayo, mara Martha akaingia…

SASA TAMBAA NAYO MWENYEWE…

“Anhaaa! Mungu kweli mkubwa.

Leo nimeamini.

Kumbe hii ndiyo biashara yenu siyo?” aliuliza Martha kwa sauti yenye kujiamini…

“Hebu kaa kwanza hapo,” alisema Roi huku akitetemeka.

Mama Anna alitetemeka lakini si sana.

Martha alivuta kiti, akakaa na kusema…

“Unasemaje wewe mwanaume mwenye majina mengi.

Maana nimesikia una majina kama matatu hivi wewe peke yako.

Kila mtu mtaani anakufahamu kwa jina lake.”

Roi alishtuka kusikia hivyo.

Kwani ni kweli mtaani ana majina mengi…

“Mh!” aliguna Roi huku akimtumbulia macho ya aibu Martha.

Lakini hakujibu hoja ya kuwa na majina mengi.

“Sikia nikwambie baby wangu Martha.

 Huyu si mpenzi wangu, ni sista‘angu ila sijawahi kukwambia,” alianza kusema Roi…

“Mimi dada yako mimi?” mama Anna alikuja juu kumuuliza Roi…

“Aaa! Jamani  dada Martha…looo! yaani unanikataa kaka yako hivihivi naona jamani?”

“We wajina…sikia, mimi si dada yake wala yeye si kaka yangu.

Mipango yetu ni kufunga ndoa.

Huyu si wa kumtegemea wewe kwani mapenzi yake ameyahamishia kwangu…we ulie tu,” alisema mama Anna kwa macho yaliyokosa aibu.

Martha alidondoka palepale, akapoteza fahamu, hali ikawa tete.

Roi huku akiogopa, alimtupia lawama mama Anna…

“Unaona sasa? Kwani kulikuwa na ulazima gani wa kumwambia wewe.

Si ningemwambia mimi mwenyewe…

“Na haikuwa lazima kumwambia sasa hivi, hata nyumbani ningemwambia…”

“Baby, mimi tatizo langu sipendi kukatishakatisha.

Niko moja kwa moja sana.

Nisamehe kwa hilo.

Ndiyo maana nilikuuliza awali unampenda nani.

Mtu akifiwa hakuna haja ya kufichaficha, ni kumwambia tu ili kama kulia alie,” alisema mama Anna.

Roi na mama Anna walimzoa Martha na kumkimbiza hospitali ambako alilazwa.

Mama Anna aliwapa taarifa wale wapangaji wengine kuhusu kuugua ghafla kwa mwenzao huyo.

***

MUDA MFUPI BAADAYE

Ilikuwa saa kumi na mbili jioni, Martha alikuwa kwake baada ya kutoka hospitali.

 Wapangaji wenzake waliingia kumpa pole kasoro mama Anna tu ambaye muda huo alikuwa nyumbani kwa Roi…

“Pole mwaya! Yaani tuliposikia umelazwa tukashangaa sana.

Da! Sasa tatizo lilikuwa wapi Martha?” mpangaji mmoja alimuuliza…

“Jamani ni hadithi ndefu sana.

lakini kifupi nilikuwa sijui kama jamaa yangu anatoka na mama Anna.

Nilihisi wakati f’lani nikafuatilia, jana usiku nikanasa meseji zao za mahaba.

“Leo asubuhi nikasema niende kazini kwake kufika namkuta mama Anna ndani.

 Yeye jamaa yangu akasema mama ni dada yake, japo nilijua ni uongo, lakini mama Anna mwenyewe akanipasulia kwamba wao si ndugu bali ni wachumba na wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni,” alitiririka Martha…

***

Kule nyumbani kwa Roi, mama Anna alimtaka Roi amruhusu awaite wale wapangaji wenzake wawili ili awatambulishe rasmi kwake…

“Aaaa…eeee…oke, waite basi,” alisema Roi ambapo awali alianza kwa kutaka kukataa.

“Mbona baby kama unasita? Au mipango yetu imekufa nini?” aliuliza mama Anna…

“Aaa! Noo…iko palepale.

Basi waite.”

Mama Anna alimpigia simu mmoja wa wapangaji wenzake, akampa maelekezo ya namna ya kufika hapo.

Wakati wanaondoka, wakamuaga Martha…

“Basi twendeni wote na mimi nataka kupeleka nguo za Roi.”

Wale ilibidi wamjulishe mama Anna kwanza ambapo naye alikubali bila kumuuliza Roi…

“Aje tu, hakikisheni amebeba hizo nguo za Roi ili asije kupata kisingizio kingine baadaye,” alisema mama Anna.

Wakati anazungumza hivyo, Roi ndiyo akasikia na kuhoji ni nini, mama Anna akamwambia, Roi akatingisha kichwa tu kukubaliana naye.

Kutoka moyoni mwake, Martha alishakubaliana na hali iliyotokea, akajilaumu sana kwa uamuzi wake wa kung’ang’ania yeye na Roi wasiwe kaka na dada na badala yake wawe wapenzi…

“Ningeusikiliza moyo siku zile haya maumivu yalikuwa yanakwepeka,”

 alisema moyoni wakiwa wanakaribia nyumbani kwa Roi yeye akiwa kiongozi maana alishafika.

Waliingia ndani watatu, wale wapangaji wawili na Martha.

Mama Anna aliwakaribisha kwa mbwembwe akijifanya mama mwenye nyumba huku Roi akionekana kukosa amani…

Karibuni jamani…karibuni sana,”

 alikaribisha mama Anna kwa sauti ya ‘mimi ndiye mmiliki halali wa mwanaume huyu’, yaani Roi sasa.

“Tunashukuru sana,” waliitikia wale wapangaji wawili kasoro Martha ambaye yeye alifikia kuweka begi chini kisha akamwambia Roi…

“Ungeangalia kama nguo zako zote zipo maana nimehakikisha siachi nguo yako hata moja.”

“Naamini zote zipo bila hata ya kuhakikisha,” alisema Roi kwa sauti iliyojaa dharau, mkono mmoja ulipita kiunoni kwa mama Anna huku mkono mwingine ukishughulika na rimoti ya televisheni.

Bila kukaa, Martha akageuza kutoka lakini kabla hajafika mlangoni, ikasikika hodi…

“Hodi,” hodi hiyo ilipigwa huku aliyepiga akisukuma mlango kuingia sebuleni.

Roi alishtuka sana, akatumbua macho huku akisimama na kusema…

“Mama Neema…mbona umekuja bila taarifa mke wangu? Umeona sasa umenikuta katika mazingira tata.

Lakini kifupi hapa hakuna mwanamke wangu mama Neema.”

PATAMU hapo,.

 Mama neema ndani ya nyumba, huku ROI akijiropokesha kwambaah.. HAPA HAKUNA MWANAMKE WAKE unadhani kwa tumfahamuvyo mama Anna atafanya je, Martha wa watu jamani anapitia wakati mgumu sana unadhani ataongea nini?!,

LOOH DADA MARTHA!

Sehemu Ya 27

ILIPOISHIA:

Kauli ya Roi ilimshtua sana mama Anna, Martha mwenyewe na wale wapangaji wawili…

“Ha! Mpenzi wangu, kumbe wewe una mke?” aliuliza mama Anna kwa sauti yenye mshtuko…

“Wewe, Mimi ni mpenzi wako tangu lini? Acha uzushi? Eti Martha, huyu mama Anna ni mpenzi wangu?” Roi aliomba huruma ya Martha ili kuokoa ndoa yake,.

Mama Neema ni mke wa Roi, Alikwenda masomoni Uingereza kwa mwaka mmoja na muda huo ndiyo alikuwa amerudi rasmi, Neema alipelekwa kusoma kwa babu yake.

“Mi mwenyewe nimeshangaa.

Kwani we mama Anna, Roi ni mpenzi wako?” aliuliza Martha huku akianza kujisikia furaha kwa anguko la mwanamke huyo aliyempindua yeye.

Mama Neema alifika kukaa kwenye kochi kubwa huku akimshangaa mume wake na ugeni ule.

Alitaka kujua…

“Baba Neema hawa wote ni akina nani na wamefuata nini hapa nyumbani?”

“Mama Neema wewe ndiyo kwanza umefika.

 Ungetulia kwanza basi, Umekuja na begi hilo moja tu?”

“Nina mizigo mingi ipo kwenye gari nje,” alijibu mama Neema kwa sauti iliyojaa hasira.

Roi alisimama na kutoka nje.

Alishusha shehena ya mizigo huku moyo ukiwa kasi.

Alijua kimenuka…

“Eti nyie ni akina nani?” mama Neema aliwauliza kwa mpigo huku akimwangalia mmoja mmoja.

“Mimi naitwa Martha, Ni rafiki wa Roi,” alisema Martha huku akiogopa.

Mama Neema akamwangalia mama Anna kama anayesema ‘na wewe?’

“Mimi naitwa mama Anna, Roi nii…niii…mimi sikujua kama Roi ana mke.”

“Nimekuuliza wewe nani, siyo Roi ana mke au hana,” alikuja juu mama Neema huku akionekana kutaka kusimama kumfuata mama Anna…

“Mimi pia ni rafiki yake wa karibu tu,” alijibu haraka mama Anna,.

Wale wapangaji wengine walijitambulisha kwa haraka huku wakisimama kutaka kuondoka.

Mizigo iliingia ndani, Roi alisaidiwa na vijana wa mtaani.

Mama Neema aliwazuia wote kutoka mpaka Roi arudi na kuzungumza naye kuhusu wao, Walikaa kinyonge.

Baada ya utulivu, Roi alirejea na kukaa…

“Baba Neema naomba utambulisho wa hawa watu wote humu ndani,” alisema mama Neema kwa sauti yenye hasira…

“Wote ni marafiki zangu, Wametoka kumoja na wataondoka pamoja.”

“Kwa nini huyu alikaa jirani na wewe kiasi kile?”

“Nani, huyu? Huyu aliamua tu.”

“Lakini mwenyewe si alisema we ni mpenzi wake?” alihoji mama Neema.

Roi alitulia akiashiria hana cha kujibu…

“Nyie malaya, nawaomba muondoke sasa hivi la sivyo nitampiga mtu risasi,” alisema mama Neema.

Akina Martha walitoka mbio, mlangoni waliminyana kila mmoja akitaka kuwa wa kwanza kutoka nje.

Wakiwa nje ya geti kuu, mama Anna alimuomba msamaha Martha…

“Martha ndugu yangu, Mi naomba nisamehe sana.

Ni kweli nilikuingilia kwenye penzi lako. Sikujua kama Roi yuko vile.

Nisamehe sana ndugu yangu.

Nimejifunza kwamba, kila binadamu na riziki yake.

Roi alikuwa riziki yako.

Mimi nikaingilia kati,” alisema mama Anna huku akimwangalia Martha…

“Mh! Yaani wewe unamwomba samahani mwenzako kwa sababu kule kumeharibika siyo? Kwa nini usingemwomba sahamani jana au juzi?”

 mmoja wa wale wapangaji aliingilia kati…

“Eti!” mwenzake alidakia.

Walimwona mama Anna kama si wao waliokuwa wakimuunga mkono na kumficha Martha kwamba wanajua.

“Sikiliza mama Anna, Kwanza sipokei msamaha wako, Pili, uache unafiki wako. Kilichokufanya uniombe msamaha ni baada ya kujua Roi kumbe ana mke.

 Usingejua je? Yaani we mwanamke mimi nimekushangaa sana, Umekuwa ukinila hivihivi najiona,” alisema kwa ukali Martha…

“Siyo hivyo Martha.

Jamani msinielewe vibaya.

Mambo mengine yanafanyika ili mtu ujifunze.

Naamini hata kilichotokea nyumbani kwa Roi kimekuwa cha makusudi ili mimi nijifunze, Please nisamehe sana Martha,” alisema mama Anna kwa sauti ya unyonge huku akimtangulia mbele na kuonesha ishara ya kutaka kupiga magoti huku akifunga mikono…

“Oke, sawa, Sasa niambie ukweli…”

“Niko tayari Martha,” alisema mama Anna…

“Wewe na Roi mmeanzia wapi na lini mpaka mkawa wapenzi?”

Japokuwa mama Anna alikuwa tayari kujibu maswali kama alivyosema mwenyewe, lakini swali hilo lilikuwa gumu sana kwake.

Ikabidi adanganye…

“Sikia Martha, Mimi na Roi tunajuana zamani sana, Tena sana, Kwa hiyo alipokuja kwako ikawa kama tunakumbushia tu,” alisema mama Anna…

“Muongo huyu Martha, Alichukua namba za simu palepale nyumbani, Siku ile wakati shemeji anatoka kuoga ndiyo akachukua, wakaanza mawasiliano.

Na alisema nia yake mpaka akupindue,” alisema mmoja wa wale wapangaji.

“Sawa jamani.

Martha ni kweli walichosema hawa.

Mimi nilijua nikikwambia hivyo utazidi kuumia wakati mtu mwenyewe haunaye tena, Nisamehe sana.”

Martha aliamua kumsamehe mama Anna huku akimwonya kutorudia tabia hiyo kwa watu wengine kwani si njema…

“Yaani kama utakuja kumfanyia hivi mtu mwingine yeyote yule, ujue maisha yako yatakuwa mabaya sana mama Anna.

Nakwambia mimi,” alisema Martha.

Wale wapangaji wengine pia wakamzodoa mama Anna na kumwambia ana tabia mbaya.

Hata wao wamejifunza kuwa naye mbali. Hata hivyo, mama Anna aliahidi kubadilika kanzia siku hiyo.

FUNZO:

UKIONA MWENZIO ANANYOLEWA ZAKO TIA MAJI,.

MWISHO.

Share.
Leave A Reply

error: Content is protected !!
Verified by MonsterInsights